WAKAZI wa eneo la Sensera Pub, Mbezi Juu jijini Dar es Salaam
wamefurika kumuona mnyama aina ya kakakuona ambaye alijitokeza juzi
usiku.
Taarifa za kujitokeza kwa mnyama huyo zilisambaa hadi chumba cha
habari cha gazeti hili ambalo lilifika eneo hilo na kushuhudia umati wa
watu ukiwa nje ya nyumba ya Martha Boniface ambaye alikuwa amemfungia
kwenye moja ya vyumba vyake vya biashara.
Martha ambaye alikuwa mtu wa kwanza kumuona mnyama huyo ambaye ni
aghalabu kuonekana, akitumika kama mtabiri wa mambo makubwa yanayoweza
kutokea katika taifa, alisema alikiona kiumbe hicho juzi saa tano usiku
kikiwa kinapita kwa mwendo wa taratibu.
“Tulikuwa tumekaa na wenzangu kama watano hapa nje jana (juzi) usiku,
mara mmoja wetu akasimama akasema jamani mdudu huyo, niliponyanyuka
nikamuona kakakuona anatembea anakuja tulipokaa, tulimpisha akasimama,
badae akajikunja, tukamnyanyua na kumuingiza kwenye boksi kumuhifadhi,”
alisema Martha.
Alisema baada ya kumuingiza kwenye boksi, walimpeleka ndani ya chumba
cha ‘stationary’ na baadae ndani ya boksi ili aweze kuzunguka.
“Usiku ule ule nilichukua maji, kisu, unga na fedha shilingi 10,000
nikamuwekea vyote kwa pamoja, maji alikunywa yote, na unga alikula wote,
fedha aliisogelea akainusa, lakini kisu alikipita akakiruka,
hakukigusa wala kukinusa,” alisema Martha.
Akielezea sababu ya kumfungia ndani ya chumba hicho, Martha alisema alilazimika kuchukua hatua hiyo ili asiondoke.
“Na usiku ule ule kabla sijafunga nikamtandikia kiroba ili asipate
baridi la sakafu, lakini asubuhi nilimkuta kalala chini,” alisema
Martha.
Kulingana na imani zilizopo nchini, kitendo cha mnyama huyo kula na
kugusa vitu hivyo vitatu kati ya vinne, baadhi wanatafsiri kuwa ni
ishara ya nchi kuwa na amani, mavuno mazuri na mvua za kutosha.
Kwa upande wake, Martha anachukulia kitendo cha kumuona kakakuona
kinatoa tafsiri ya neema na bahati ambayo ameshushiwa na Mungu kwani
kiumbe huyo huonekana mara chache.
MTANZANIA Jumapili lilishuhudia baadhi ya wananchi waliofika katika
eneo hilo kwa nia ya kukishuhudia kiumbe hicho wakishikwa na mshangao
wakati Martha akijaribu kukibembeleza kijikunjue katika gamba lake
analolitumia kujificha ili kiweze kuonekana vizuri.
“Mgeni naomba uamke uwasalimie wenyeji wako wamekuja kukuona, tunajua
umekuja kwa nia nzuri, umetuletea baraka, lakini watu wanatamani
kukuona, naomba ujifungue ili uwasalimie wenyeji wako,” alisikika
akisema Martha wakati akijitahidi kukifanya kiumbe hicho kijikunjue.
Baada ya muda kakakuona alianza kufungua miguu yake yote na kisha
mkia, na baadae akaanza kutembea akizunguka huku na huko ndani ya chumba
hicho.
Aidha mmoja wa jirani wa eneo hilo, Syntyche Sanya, alisema kwa mara
ya kwanza alimuona kakakuona katika eneo hilo Jumatano asubuhi wakati
anaenda kazini.
“Mimi nilimuona saa 11 alfajiri wakati naenda kazini, kwa sababu
nilikuwa simjui sikumfuatilia kabisa, nikajua ni mnyama wa kawaida,”
alisema Sanya.
Mume wa Martha, Boniface Machera, alisema amefurahishwa na ujio wa
myama huo mtaani kwao, lakini kutokana na umuhimu wake, waliamua
kumuhifadhi hadi watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii
watakapokuja.
“Tumemuhifadhi kwa sababu akiondoka kuna mawili, anaweza akapotea au watu wakamkamata na kumtoa magamba,” alisema Machera.
Aidha baadhi ya vijana waliofika kumuona kakakuona, walitumia tukio hilo kufanya utani.
Mmoja wa vijana hao alisikika akisema: “Tumemuwekea bendera mbili, ya
CCM na Chadema, lakini akaenda kuegemea ya Chadema,” alisema huku
wenzake wakiangua kicheko.
Hata hivyo, alipoulizwa Boniface kuhusu taarifa hizo, alicheka na
kusema kuwa walikuwa wanatania tu na hakuna bendera yoyote iliyowekwa.
Mara ya mwisho mnyama huyo alionekana jijini Dar es Salaam Julai mwaka
jana katika eneo la Buza na mwaka huu ni mara ya kwanza kujitokeza.
Alionekana pia Oktoba mwaka 2010 katika eneo la Bunju ambako wananchi
walimuwekea nafaka, silaha za jadi, maji na vitu vingine, lakini
alienda kuegemea panga akiashiria hatari.