Katika kipindi cha magazeti asubuhi leo kupitia redio Saut Fm ya Mwanza baadhi ya magazeti yameripoti kitu kisicho cha kawaida.

Rais wa Marekani Mh.Barack Obama amemtaka Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete kueleza juu ya udokozi na uchukuaji wa fedha katika akaunt ya ESCROW.

Ikumbukwekwe kuwa hapa nchini wabunge walielezea juu ya wizi huo ila baadhi yao wameishia kushtakiwa mmoja wao ni KAFULILA.

Mambo yamekuwa mambo "There is no parmanent friend nor enermy" USA slogan.



OBAMA KUMGEUKA KIKWETE?



Aulizia mradi wa IPTL, Wahisani waweza kugomea misaada


Mwandishi Wetu
RAIS Barack Obama wa Marekani amemuuliza Rais Jakaya Kikwete kuhusu fedha za kampuni ya kufua umeme ya IPTL zilizochukuliwa kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Raia Mwema limeambiwa.

Gazeti hili limeelezwa kwamba Obama alimuuliza Kikwete kuhusu suala hilo wakati wa Mkutano wa Viongozi wa Bara la Afrika na Marekani uliomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita nchini humo.

Marekani inaelezwa kutofurahishwa na namna Tanzania inavyolishughulikia suala la IPTL, ambalo limekuwa likitajwa kuhusika na rushwa tangu kuingia kwa kampuni hiyo hapa nchini takribani miaka 20 iliyopita.

“Obama alimuuliza Kikwete kuhusu IPTL na kwamba kwanini hadi leo watu wanaotajwa kuhusika na rushwa katika suala hilo wameachwa.

“Kwa bahati nzuri, zilikuwepo ripoti mapema kwamba huenda Obama au Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, John Kerry, angeweza kuibua suala hilo na hivyo tunadhani Kikwete alitoa majibu mazuri,” kilisema chanzo kimoja cha gazeti hili nchini Marekani ambacho kilifuatilia Mkutano huo wa Obama na marais wa Afrika kwa karibu.

Raia Mwema halikuweza kubaini ni majibu gani ambayo Kikwete aliyatoa kwa Obama, kwa vile inadaiwa mazungumzo yao yalikuwa ya wawili tu na kwamba taarifa zimepatikana kwa sababu suala hilo lilikuwa limezungumzwa na wasaidizi wa Obama.

Hadi tunakwenda mitamboni, juhudi za kuwapata wasemaji wa Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuthibitisha taarifa hizi hazikuweza kufanikiwa.

Kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 200 zinadaiwa kuchotwa kutoka katika akaunti ya Tegeta Escrow ambako fedha hizo zilikuwa zimehifadhiwa kwa sababu ya mgogoro uliokuwapo baina ya Tanesco na IPTL.

Akaunti hiyo ya Tegeta ilikuwa na jumla ya dola za Marekani milioni 250 zilizokuwa zimehifadhiwa, na kwa sababu ya kuchukuliwa kwa dola 122 za kwanza, sasa imebaki na dola milioni 128 tu.

Tanesco walikuwa wanadai kwamba IPTL ilifanya vitendo vya uvunjaji wa mkataba na kutaka mkataba wao uvunjwe, katika mojawapo ya uwekezaji wenye utata katika historia ya Tanzania.

Tangu mradi wa IPTL uanze yamekuwepo madai ya vitendo vya rushwa miongoni mwa watumishi wa serikali ili kuruhusu mradi huo uendelee na inaelezwa hiyo ndiyo sababu Obama aliuliza kuhusu suala hilo.

Raia Mwema linafahamu kwamba ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeanza kulichunguza suala hilo la kuchukuliwa kwa fedha za akaunti ya Tegeta.

Tayari baadhi ya viongozi wa serikali pamoja na wabunge wamehojiwa na CAG kuhusu suala hilo na inatarajiwa kwamba uchunguzi unaweza kukamilika kabla ya Septemba mwaka huu.

Suala la rushwa ni muhimu kwa Marekani kwa sababu mojawapo ya vigezo vya nchi kupata msaada kupitia Mpango wa Changamoto za Milenia (MCC) ni nchi kutokuwa na rushwa.

Tanzania ilifaidika na Awamu ya Kwanza ya Mradi wa MCC ulioipatia kiasi cha dola milioni 698. Awamu hiyo imemalizika mwaka jana.

Mwaka huu, Tanzania imeomba pia kuwemo katika Awamu ya Pili ya mgawo wa MCC, na tayari serikali imetenga sehemu kubwa ya fedha hizo kwenye miradi ya umeme wa vijijini.

Kabla ya Rais Kikwete kwenda Marekani, Watanzania wanaoishi nchini humo na ambao wako karibu na duru za utendaji za serikali hiyo, waliandika waraka kwa Rais Kikwete kumweleza namna suala la rushwa lilivyo muhimu kulieleza vizuri.

Vyanzo vya gazeti hili kutoka Marekani vimeeleza kwamba serikali ya Marekani ingependa Tanzania isonge mbele katika mapambano dhidi ya rushwa kwa vile tangu Awamu ya Kwanza ya MCC, nchi imeshuka katika vigezo vya kupambana na rushwa.

“Wakati Tanzania ikipata misaada ya MCC katika Awamu ya Kwanza ya Kikwete, nchi ilikuwa imepata alama 80 katika viwango vya rushwa. Hivi sasa Tanzania imeshuka hadi alama 50 jambo ambalo ni la hatari.

“Kwa kawaida, nchi yoyote ambayo alama zake zimeshuka kufikia nusu ya kiwango cha awali, inajiweka katika hatari ya kukosa misaada ya MCC. Tanzania ijitazame sana kwenye hili,” kilisema chanzo hicho ambacho kwa sababu za wazi kabisa hatutaweza kukitaja.

Kwa mujibu wa ratiba ambayo gazeti hili imetumiwa kutoka Marekani, Bodi ya MCC inatarajiwa kukutana Septemba mwaka huu kwa ajili ya kupitisha majina ya nchi zitakazonufaika na Awamu ya Pili ya MCC na ndiyo maana ni muhimu uchunguzi wa CAG ukamalizika kabla ya wakati huo.

CHANZO: Raia mwema




UPDATE



IKULU YAKANUSHA JK KUHOJIWA NA OBAMA


MKURUGENZI wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu amekanusha madai yaliyotangazwa hivi karibuni kwamba, Rais Jakaya Kikwete amehojiwa na Rais wa Marekani, Barack Obama, kuhusu fedha za kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam jana kukanusha taarifa hizo zilizotolewa na moja ya gazeti la kila siku nchini, (si Habarileo), Rweyemamu alisema katika ziara ya Rais nchini Marekani hivi karibuni, hakukutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Obama.
Kwa mujibu wa Rweyemamu, katika ziara hiyo ambayo Rais Kikwete alihudhuria Mkutano wa Viongozi wa Bara la Afrika na Marekani, alikutana na Mkurugenzi mpya wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).

“Rais pia alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na katika mikutano yote hiyo hakuna jambo lolote linalohusu IPTL lililojadiliwa wala kuulizwa.

“Huu ni uongo na ni habari ya kutungwa na habari kama hizi huandikwa kwa ajenda, sasa sijui hawa wenzetu waliandika kwa ajenda zipi,” alifafanua.
Alisema masuala yote yanayohusu kilichojiri katika mkutano huo na namna Tanzania ilivyonufaika katika sekta mbalimbali, yatabainishwa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Hoja ya kuchukuliwa kwa karibu Sh bilioni 20 IPTL katika akaunti ya Escrow iliyokuwa BoT, iliwasilishwa bungeni hivi karibuni na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), akidai kuna wizi umefanyika.

Kutokana na hoja hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa ufafanuzi kwamba uamuzi wa kuingiza takribani Sh bilioni 20 katika akaunti ya Escrow, haukuwa wa kificho kwa kuwa fedha hizo zilikuwa za IPTL na zilitolewa na kukabidhiwa kwa kampuni hiyo ya kufua umeme, kwa uamuzi wa Mahakama.

Alifafanua kuwa suala la IPTL ni la muda mrefu tangu 1994, wakati huo Serikali baada ya kuona lipo tatizo la umeme, ilitafuta mtu aliyekuwa tayari kuzalisha umeme.

Mkataba ulionesha umeme utakaozalishwa utauzwa katika Shirika la Umeme (Tanesco) na ulikuwa na sehemu mbili kwa maana ya malipo ya uwepo wa mtambo na pia uzalishaji.

Wakati wakiendelea kuzalisha umeme, Pinda alisema kulitokea mgogoro upande wa Tanesco na IPTL, kuhusu kodi inayopaswa kulipwa na baadaye ukazaa kesi iliyopelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.

Wakati mgogoro huo ukiendelea, Pinda alisema Serikali ililazimika kufungua akaunti ya Escrow na fedha kutoka Tanesco zikawa zikilipwa kwenye akaunti hiyo.

Alisema fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti hiyo, ni za IPTL na katika uamuzi wa Mahakama ikaamriwa fedha hizo zipelekwe IPTL kwa kuwa ni fedha zao.

“Fedha hizo zikapelekwa IPTL, jambo tunalopaswa kama wabunge kujiridhisha nalo ni je, VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ipo kweli au haipo?,” alisema Pinda.

Alisema baada ya kesi kumalizika, Tanesco na IPTL walikaa wakatazama kiasi kinachodaiwa, wakafika mahali wakakubaliana ni kiasi gani cha fedha kilipwe. Alisema kwa upande huo, kama kuna masuala yanaweza kupatiwa majibu bila mjadala na kuvutana.

“Kubwa ni pale zogo limejikita zaidi kwenye kuondoa fedha kutoka akaunti ya Escrow kutoka Benki Kuu kupeleka IPTL na maswali ambayo yamejitokeza kwamba kodi haikulipwa, ufisadi upo, unajiuliza wa nini kama fedha ile ilikuwa ni fedha yao,” alihoji Pinda.

Kutokana na hali hiyo, Pinda aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuchunguza na kujiridhisha kama kweli upo uchotaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti hiyo, uchunguzi ambao matokeo yake hayajatoka mpaka sasa.